Ndugu yangu mmoja (shemeji yangu) hupenda kunukuu maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere miaka ya mwanzo wa uhuru kuhusu Taifa na Utaifa. Kwamba kuna masuala ambayo mtu akiyafanya hata awe ni Rais watu waweze kusema ‘huu sio Utanzania’ (wakati huo Utanganyika). Hupenda kusisitiza pale Mwalimu aliposema ‘watu wakatae awe ‘President or President squared’. Wakati tunaanza siku ya kwanza ya kutafuta miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika, nimetafakari kama tumeweza kujenga Taifa ambalo tunaweza kutafsiri maneno na matendo ya mtu kama ‘sio Utanzania’ hata yakisemwa na mtu mwenye mamlaka kiasi gani. Mjadala wa aina hii hivi sasa katika zama za rasimu ya Katiba na Katiba inayopendekezwa huitwa ‘tunu za Taifa’.
Mwalimu na wenzake walikuwa na kazi kubwa ya kulisuka Taifa kutoka kwenye mkusanyiko wa makabila. Ilibidi kutafuta itikadi moja ya kitaifa ambayo kupitia kwayo mfumo wa tunu za kitaifa (national values system) ulijengwa. Huu ni mfumo wa kanuni na desturi za maisha na malengo ya kijamii ambazo kwa wastani kila mwana jamii anaziamini kwa hiari au kwa ‘lazima’. Kiufupi ni kanuni za ‘masuala sahihi (right) ’ na ‘masuala yasiyo sahihi (wrong)’ yaliyokubalika katika jamii. Kusuka Taifa kutoka kwenye makabila zaidi ya 120 yenye tunu zao, na kujenga tunu za watu wote, sio jambo jepesi na sio lelemama. Hata hivyo kupitia Elimu ya Taifa na oganaizesheni ya Chama cha TANU ikiwemo Jeshi la Kujenga Taifa waasisi walifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Ilifika wakati, mtu kutamka lugha za kibaguzi hadharani ilikuwa sio Utanzania. Wizi wa mali ya umma ilikuwa sio Utanzania. Uzembe makazini ulikuwa sio Utanzania. Kila Mtanzania alikuwa ana uhakika kwamba ‘atatambuliwa na kuthaminiwa utu wake’. Itikadi ya Ujamaa iliweka msingi mkubwa wa kuhakikisha kuwa watu wanakuwa sawa mbele ya sheria na kila mtu anawajibika ipasavyo. Lugha ya Kiswahili ilisaidia sana kuunganisha Taifa na kuweka wazi kinachoitwa ‘national identity’. Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja wa Taifa na Uwajibikaji haviakuandikwa kwenye Katiba lakini viliingia kwenye mishipa ya damu za Watanzania kiasi kwamba aliyekwenda kinyume chake alionekana sio Mtanzania. Sio kwamba hawakuwepo, walikuwepo wengi sana lakini mfumo ulijengwa kwa namna ya kwamba wakigundulika wanashughulikiwa kisheria, kisiasa na hata kijamii.
Miaka ya hivi karibuni hali imebadilika. Wakati mwingine unajiuliza ndoto za Taifa hili ni nini? Ninaweza kusema bila woga kuwa wakati ninakua nilifunzwa kuwa ndoto ya Tanzania ni ‘kuwa na jamii ya watu walio sawa na huru’ ambapo tuliambiwa ili kufikia jamii hiyo ‘ Ujamaa na Kujitegemea ni njia pekee’. Kutokana na mabadiliko katika dunia inawezekana Ujamaa sio njia pekee tena bali kuna njia nyingine mbadala. Lakini hizo njia nyingine zinatufikisha kwenye ndoto hiyo?
Hivi sasa mwanasiasa yeyote anaweza kusimama popote na kutoa lugha za kibaguzi na akashangiliwa. Wabadhirifu wa Mali ya Umma ndio wajanja. Wazembe wanaopelekea mabilioni ya fedha za Umma kupotea/kuibwa/kuchotwa ndio wazalendo. Wawekezaji makanjanja wanalindwa. Raia hawaheshimu tena dola na kuamua kumalizana wenyewe kwa wenyewe na tunaaminishwa ni vita ya wakulima na wafugaji kugombea ardhi. Ilhali wageni wametwaa maelfu ya ekari za ardhi na wanalindwa na askari wanaoendeshwa kwa kodi za hao hao wakulima na wafugaji wanaouana. Lugha ya Kiswahili bado ipo lakini hakuna itikadi inayounganisha Watanzania tukaweza kusema ‘ huu sio utanzania’. Ndoto ya Taifa hili tunayoirithisha kutoka kizazi kwenda kizazi haipo na juhudi za kuweka tunu Fulani kwenye Katiba zimepigwa vita. Tunakuwa kama kundi la kondoo wasio na mchungaji. Iwapo Tunu za Taifa zingekuwapo mchakato wa katiba usingebaki wa upande mmoja, maridhiano yangepatikana.
Unapoona Taasisi za Dola zinapingana kwenye jambo lililowazi ujue Dola hiyo haina muda mrefu itaporomoka. Unapoona vyombo vya Dola vya Nchi vinasema hivi na wanasiasa kwa kutumia mamlaka yao wanasema vile ujue Taifa hilo linakwenda kufa. Taasisi na Dola na vyombo vya Dola kugongana yaweza kuwa ni afya ya demokrasia. Lakini vinapogongana katika kulinda wizi na ubadhirifu yaweza kuwa ni kansa ya demokrasia. Kansa ya demokra
Unapoona Taasisi za Dola zinapingana kwenye jambo lililowazi ujue Dola hiyo haina muda mrefu itaporomoka. Unapoona vyombo vya Dola vya Nchi vinasema hivi na wanasiasa kwa kutumia mamlaka yao wanasema vile ujue Taifa hilo linakwenda kufa. Taasisi na Dola na vyombo vya Dola kugongana yaweza kuwa ni afya ya demokrasia. Lakini vinapogongana katika kulinda wizi na ubadhirifu yaweza kuwa ni kansa ya demokrasia. Kansa ya demokra
sia ‘sio Utanzania’.

0 comments:
Post a Comment